0





 UKIWA na mtu mpende kwa dhati hadi aone kweli wewe unamaanisha kumpenda, siyo vinginevyo.
Kumpenda mtu kwa dhati, kunasaidia kumfanya ajione wa maana katika maisha na hiyo inasaidia kuondoa kasoro mbalimbali zikiwamo za kufanya ngono nje ya ndoa.

Ukweli ni kwamba, ikiwa kweli unataka maisha mazuri ya ndoa ni lazima kujifunza namna ya kupendana kwa dhati na kuacha unafiki kama walivyo baadhi ya watu.
Msingi wa maisha yanayofaa ni kuona kama mnaendana. Ukiona kama hamuendani, siyo sahihi kuulazimisha moyo.
Hili nalisema hasa kwa wale ambao bado hawajaoana. Kwa walio kwenye ndoa, kama kunatokea kutoelewana, cha msingi ni kuzungumza, kwa sababu kuachana ni jambo baya, linalosumbua hata watoto na kuharibu mfumo wa maisha kwa jumla.
Tunaishi katika ulimwengu, ambao makosa ni mengi. Kwa maana hiyo, siyo sahihi hata kidogo kufikiria kuachana badala yake angalia namna gani mnaweza kwenda sawa.
Mkipendana na kuonyeshana huruma kwenye uhusiano au ndoa, ndipo mtakapoishi na kupata faraja.
Je, mpenzi wako unamchukuliaje?
Kila mtu anaweza kujibu swali hilo kadri anavyotaka. Wengine wake zao ni wafanyakazi wa ndani, hawana mamlaka ya kuuliza kuhusu biashara wala kipato; hii siyo sahihi.
Kwa wapenzi, kutopendana au kutohurumiana huwa ndiyo msingi wa kuharibika kwa kila kitu katika maisha yao. Ndiyo kusema, ni jambo muhimu zaidi kwa kila mtu aliye katika uhusiano, kufikiria mbinu za kufanya, ili kumpenda zaidi mwenzi wake.
Lakini kwa sasa kwa kweli hali siyo ya kufurahisha sana. Kuna nyumba nyingine, mwanamke akiwa mjamzito, hapo ni tiketi ya mwanamume kwenda nje ya ndoa na kuanza kudharau familia.
Kuna wanaume wengine kwa sababu yeye ni mwanamume, hata kama mke anaumwa vipi, hayuko tayari kusaidia hata kupika au kuchota maji. Hii siyo sawa hata kidogo. Wengine ndiyo kwanza anaondoka kabisa nyumbani. Upendo ni kusaidiana na kuhurumiana.
Maisha ya kweli yenye furaha ni pamoja na kuangalia namna gani ufanye, ili kuishi kwa amani na yule uliye naye.
Yeyote ambaye anaishi kwa jeuri na mkewe au mumewe, ajue kwamba anajitafutia mikosi mwenyewe katika maisha yake.

Ni vigumu kufanikiwa, wakati watoto wanalia labda wameshindwa kupelekwa shule nzuri au wanaishi kwa shida, eti baba anahangaika na wanawake wengine nje ya ndoa.


TOA MAONI YAKO

 

Post a Comment

AddThis

 
Top