0
UMEONA wachambuzi na wadau wengi wa habari wameandika kuhusiana na tathimini ya namna ulivyokuwa mwaka 2014 na matokeo yake kibao katika michezo mbalimbali.


Wamesema kocha alivyofukuzwa, wameeleza makocha wapya walivyoajiriwa, namna timu zilivyosajili wachezaji wapya, migogoro kwenye vyama vya riadha na kadhalika.

Mambo ni mengi, unaweza kuyaita burudani ya kutosha lakini ukweli hasa ni yale yanayoonyesha katika mwaka huu tunaoumaliza leo hakuna la maana ambalo tulilifanya na tunaweza kujivunia.

Tumefanya nini kwenye kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars? Tumefanya nini kwenye timu ya taifa ya wanawake, Twiga Stars? Jibu litakuwa hakuna. Hata kama utauliza kwenye ngumi za kulipwa, ridhaa, riadha, zaidi ya afadhali, hakuna cha kujivunia kwamba kilikuwa kikubwa na kitakuwa dira au muongozo sahihi kwa mwaka unaoanza kesho wa 2015.

Leo ndiyo siku ya mwisho ya mwaka 2014, mwaka ambao haukuwa na tija hasa katika soka na michezo mingine. Mimi niufunge kwa masikitizo makubwa na hasa katika suala la Nani Mtani Jembe.

Nimekuwa nikihoji mara kadhaa kuhusiana na klabu za Yanga na Simba, kwamba zilifaidika nini wakati wa mechi ya kirafiki iliyopewa jina la Nani Mtani Jembe kwa kuwa tuliona idadi kubwa ya watu iliyojaa uwanjani.

Hakuna ubishi idadi ya mapato, unaweza kukadiria hadi Sh milioni 550 lakini uchanganuzi wa mapato kuhusiana na mechi hiyo umekuwa ni kama kiza. Kimya kutoka TBL ambao ndiyo wanaomiliki Bia ya Kilimanjaro inayozidhamini Yanga na Simba.

Maswali yote ya msingi hayajajibiwa, badala yake chuki na hasira kwa baadhi ya wahusika kuwa kwa nini ninahoji! Lakini si suala la chuki, badala yake ni maswali ya kawaida anayoweza kuuliza yeyote anayejiuliza na anayetaka kujifunza.

Najua wako waliokaa kimya, watu wa hewala, wasiojali wapi tunakwenda kombo au wasioona haja ya kurekebisha upepo mbaya kabla haujatengeneza dhoruba inayoweza kuuvuruga kabisa mchezo wa soka ambao bado unasuasua.

Wapo mashabiki wa soka ambao wamekuwa wakiniunga mkono tena sana kwa kuchangia kupitia simu yangu ya maoni yenye namba 0658 939769.

Wengine siwajibu, waniwie radhi kwa kuwa ujumbe unaoingia ni mwingi kupita kiasi, nahitaji muda wa ziada hata kuwaambia nawashukuru kwa kuelewa nini ninachokihoji, ni kwa ajili ya manufaa ya mchezo wa soka.

Hakuna anayeweza kukataa fedha za viingilio siku hiyo zilitolewa na wapenda mpira nchini ambao wangependa mpira uendelee kupitia fedha zinazotokana na mchezo huo. Nisisitize, Simba na Yanga si mali ya viongozi wa klabu hizo, badala yake wanachama, hivyo wana haki ya kujua.

Taarifa zinaeleza Kilimanjaro ndiyo waliandaa pambano hilo, sawa. Ingawa mimi najua kazi kubwa ya kampuni hiyo ni utengenezaji wa ‘udirinki’, vipi iingie hadi kwenye kuandaa masuala ya mechi? Vipi wachukue hadi mapato wakati wao ni wadhamini na walipaswa kufaidika na udhamini tu?

Ukimya wao unazua maswali mengi sana. Kwanza niwaahidi sitachoka, nitaenda nikiwashirikisha hadi mashabiki wa Yanga na Simba, siku watakayofunguka na kuweka ukweli hadharani, nitakaa kimya.

Kikubwa watueleze, wao TBL kama ni kweli walichukua fedha, kiasi gani na kwa nini? kama si wao, aliyechukua ni nani, kiasi gani na kwa nini?

Ukimya huu maana yake mapato hayo yamepotea hewani au kuna watu wamegawana. Je, kama waliogawana hawaoni kama wataichafua TBL ambayo kiheshima iko juu kwa maana ya moja ya makampuni makubwa nchini?

TBL ikiendelea kukaa kimya, kumbe haijachukua haioni inajichafua? Kama yupo aliyechukua na kuziacha Yanga na Simba zikiwa hazina kitu haoni ni kuzidi kuzinyong’onyesha na kuzitumia mwisho kuziacha zikiendelea kuogelea umasikini?

Maswali yako mengi, yanapaswa kujibiwa badala ya ukimya ambao hauna sababu. Safari ijayo, nitakuja na maoni ya mashabiki wa soka ambao wamekuwa wakinitumia ujumbe wao, nawasisitiza waweke tu majina yao na waniambie wako tayari nitumie walichokiandika na namba zao za simu.

Naufunga mwaka huu na maswali mengi ya kujiuliza. Bado nasisitiza hivi, kwa kuwa nina haki ya kuhoji kama chombo cha habari, basi nitaufungua mwaka na maswali zaidi, hadi kitakapoeleweka. Wadau kila la kheri na mwaka wa 2015.

Post a Comment

AddThis

 
Top