Sina haja ya kurudia kuelezea kuhusu ubora wa kazi zake, kwa sababu kama ni kuimba, anajua.
TID, licha ya umaarufu wake, ameendelea kuishi maisha yake yaleyale ya uswahilini na mpaka miaka ya hivi karibuni, alikuwa bado anaishi nyumbani kwao, mitaa ya Kinondoni. Mara kibao utamkuta ametulia maskani, akiwa na washkaji wa miaka yote, tofauti kabisa na baadhi ya mastaa ninaowajua, ambao umaarufu uliwahamisha na kuwatenganisha na watu wao wa zamani.
Mara kadhaa aliwahi kunialika kushuhudia mazoezi ya bendi yake ya Top Band na hata katika baadhi ya shoo. Ukaribu wangu na TID ulianza kupungua baada ya umri kunilazimisha kupunguza mitoko.
Zamani tungeweza kukutana kila siku katika kumbi za starehe, lakini mwili wangu umeanza kuchoka, hivyo ni bora kuuheshimu ili angalau nisogeesogee kidogo!Baada ya kama miaka miwili au mitatu ya kuongea tu kwenye simu, tena mara chachechache, nilimuona katika Kipindi cha Sporah Show kupitia mtandao.
Dah, mchizi wangu alikuwa amepungua kidogo na aina ya maswali aliyokuwa anaulizwa na mwendesha kipindi na majibu aliyokuwa anatoa, yalionyesha kuwapo kwa tatizo.Lakini yapata miezi kama saba hivi iliyopita, nilikutana ana kwa ana na TID, siku niliyoenda kuosha macho Nyumbani Lounge, kwenye shoo za kila Ijumaa za Machozi Band ya Lady Jaydee.
Ninamfahamu huyu jamaa kama nilivyosema, alikuwa amebadilika, amepungua!
TID ni mtoto wa mjini, si mnakumbuka aliwahi kumdunda jamaa hadi akafungwa? Sikuwa na ujasiri wa kumuuliza kulikoni, lakini nikadhamiria kuchunguza nini kimemtokea rafiki yangu. Uchunguzi wangu ulikuwa ni kwa kuwatumia wasanii wenzake.
Wenzake wanasema TID anatumia kilevi hatari. Najua maandishi haya yanaweza kumaliza kabisa uhusiano wetu, lakini kwa kuwa nina dhamira njema, sijali. Binafsi ninaamini rafiki ni yule anayekueleza ukweli, ili kama vipi uchukue hatua.
TID, mimi ni mtoto wa mjini kama wewe. Tofauti yetu kubwa ni kwamba wewe unapata hela na fursa nyingi kuliko mimi, ingawa kiumri mimi ni kaka yako. Ninavyojua, watoto wa mjini huwa wajanja na sifa kubwa ya mjanja ni kujitambua, yeye ni nani, anafanya nini, kwa ajili ya nini na hata kujua kesho yake iko vipi.
Kilevi unachokitumia, hakijawahi kumnufaisha mtu yeyote, maana historia inaonyesha kila aliyeshiriki, hata akiwa tajiri vipi, aliishia kuwa maskini na wengine hata kufa kwa msongo wa mawazo. Kama ulikitumia ili kukidhi vigezo vya kula ujana, sema yatosha, achana nao!
Ni jambo la kusikitisha sana, kuona mmoja kati ya wasanii wenye mashabiki wengi, anajimaliza kwa kitu ambacho hakina umuhimu wowote katika maisha, zaidi ya kummalizia hela na kumwondolea heshima mbele ya jamii.
Hujachelewa, amua kuacha na jamii itakusaidia. Unaweza kuwaona wanaokushauri kama washamba na wanaofuatilia maisha yako, lakini mwisho wa siku wanafanya hivyo kwa faida yako mwenyewe. Kitu kimoja nataka ukijue, unapokatiza huku mtaani, watu wanaonyeshana vidole, halafu wanasema “Dah, mwone TID alivyochonga.”
Post a Comment