Nahodha wa timu ya Mbeya City, Mwigane Yeya ambaye yupo katika kambi ya timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars amesema kuwa imani ni kubwa kwa timu yao kuwa wanaweza kutwaa ubingwa wa ligi kuu Tanzania Bara msimu huu. City ilimaliza katika nafasi ya Tatu msimu uliopita na sasa katika msimu wake wa pili wa ligi kuu timu hiyo imekuwa pekee ambayo haijaruhusu bao miongoni mwa timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo.
“ Ligi ni ngumu msimu huu, nachoweza kusema ni kuwa kila mechi imekuwa ngumu na ushindi hauji kiurahisi kwa sababu kila timu inaoneka kufanya maandalizi ya kutosha. City imejipanga kufanya vizuri zaidi ya msimu uliopita, kutwaa ubingwa ni sehemu ya malengo yetu msimu huu” alisema mchezaji huyo wakati alipozungumza na mtandao huu.
City ililazimishwa suluhu-tasa na JKT Ruvu ya Pwani katika uwanja wa Sokoine kabla ya kuichapa Coastal Union kwa bao 1-0 katika mchezo wa pili ndani ya uwanja wa nyumbani na mwishoni mwa wiki iliyopita walilazimisha suluhu-tasa dhidi ya Ruvu Shooting katika uwanja wa Mabatini, Mlandizi, Pwani. City wanashika nafasi ya nne nyuma ya Yanga, AZam FC na Mtibwa Sugar
Post a Comment