Patrick Phiri amekubali kujiunga na moja ya klabu kubwa na ya muda mrefu nchini, Simba SC , lakini hilo limekuja kufuatia kufutwa kazi kwa kocha, Mcroatia, Zdravko Logarusic mapema siku ya Jumatatu. Kwa mtazamo wa kawaida wa kimpira, uamuzi huo unaonekana kuwa mzuri kwa kila upande.
Phiri raia wa Zambia hakuwa na mafanikio ya kujivunia tangu alipoachana na Simba, mapema mwaka, 2011 baada ya kumalizika kwa mkataba wake wa miaka mitatu. Kitu ambacho kilikuwa wazi ni kufukwa kazi kwa Loga, lakini uongozi wa Simba umetumia muda mfupi kumtangaza Phiri kama kocha ambaye atarithi nafasi hiyo ambayo imekuwa chini ya walimu watano tofauti katika kipindi cha misimu mitatu iliyopita.Simba imeshindwa kumaliza katika nafasi mbili za juu katika ligi kuu ya Tanzania Bara katika misimu miwili iliyopita. Walimaliza katika nafasi ya tatu msimu wa 2012/13 na walikuwa washindi wa nne msimu uliopita.
Kwa hali yoyote timu hiyo ipo katika kipindi kigumu inawezekana isifikie ugumu wa miaka ya 1996-2000 waliposhindwa kutwaa ubingwa kwa miaka minne mfululizo ila kwa mtazamo wa kawaida ni kwamba timu hiyo imekosa makali. Kwa nini imekuwa hivyo?. Je, Phiri atakuja na ujuzi gani mpya ambao utaisimamisha timu hiyo?.
Kuna matatizo mengi katika timu hiyo na inawezekana makocha, Moses Basena, Milovan Curkovic, Patrick Liewig, Abdallah King Kibadeni, na Loga walikuwa na ujuzi mdogo lakini si wote walikuwa huru kufanya kazi yao chini ya uongozi uliopita ambao ulitawaliwa na migogoro ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka miwili ya mwisho. Ni jambo la kuvutia kumuona, Phiri akirejea Simba kwa mara nyingine, lakini hatafanikiwa kama ataendelea kubughudhiwa katika utendaji wa kazi kwa kushinikizwa baadhi ya mambo ya ufundi katika timu.
Suleimani Matola hakuna shaka kuwa ataendelea kufanya kazi kama kocha msaidizi klabuni hapo, Phiri ni aina ya kocha ambaye Simba ingependa kuwa naye, na Simba ni timu ambayo pia Phiri angependa kuifundisha. Lakini kama mambo yaliyo muondoa miaka ya 2005 na 2011 hayatarekebishwa, mipango mingi itaharibika na mpango wa klabu na mwalimu hautafanikiwa.
Kwa upande mwingine Phiri amekuwa kocha mwenye mafanikio makubwa katika ufanyaji wake wa kazi klabuni hapo, hivyo alitazamwa haraka kama mtu sahihi wa kuinyanyua timu hiyo kutokana na kuifahamu kwake ila ni mambo mengi atalazimika kupambana nayo kwenye uongozi wa klabu. Kuna mambo mengi yanaleta presha katika soka la Tanzania, kama mwalimu unapewa kazi na hautafanya vizuri unawajibishwa , hivyo mpango wa kwanza sahihi wa kumsaidia Phiri kuvuka kigingi hicho ni kuipa matokeo ikiwezekana kushinda ubingwa japo hakuna hatakayehoji sana ikiwa timu itafanikiwa kupanda hadi katika nafasi ya pili.
Jambo hilo litakuwa gumu kwa Phiri lakini ni lazima ahakikishe anajianda kushinda. Hilo ni jambo ambalo anaweza kupambana nalo. Hakuna shaka kuwa Zacharia Hans Poppe, Geofrey Nyange Kaburu na Evance Aveva ni watu wenye nguvu katika uongozi wa Simba, na pia Phiri atakuwa amezungukwa na wachezaji wengi wa zamani katika benchi la timu hiyo ambao watakuwa katika majukumu mbalimbali, lakini wengi wao hawana aibu na huweka hisia zao wazi pindi mambo yanapokwenda hovyo. Hicho ndicho kitu kinachofanyika Simba kwa miaka nenda, rudi.
Watu hao ni muhimu sana kama watakuwa upande wako kukusapoti, lakini huwa hatari pia wanapokuwa wakipingana na mbinu za mwalimu. Kama, Phiri atashindwa kuanza msimu ujao vizuri, bila shaka atakutana na mambo mengi ambayo yatamyumbisha mbele yake. Misimu mitatu iliyopita Simba ilikuwa katika nafasi nzuri ya kiushindani barani Afrika, lakini kitendo cha kuondoka kwa Phiri timu hiyo ilianza kuporomoka taratibu kabla ya kutokomea hadi katika soka la ndani.
Sidhani kama kulikuwa na haja yoyote ya Simba kumfuta kazi Loga, ila kulikuwa na sababu muhimu iliyofanya hilo kutokea ikiwemo kitendo cha kocha huyo kumtukana, mchezaji Shaaban Kisiga katika vyumba vya kubadilishia nguo siku ya Jumapili iliyopita wakati wa mchezo wa hisani dhidi ya Zesco ya Zambia. Loga alikuwa ni mtu anayelalamikiwa sana na wachezaji lakini wachezaji wengine wamekuwa na matatizo sugu ya kutowaheshimu walimu wao kwa sababu ya kusajiliwa na viongozi.
Kama Simba wataendelea kufanya kama walivyofanya litakuwa ja,mbo gumu kwao kujinasua, lakini uamuzi wa Phiri kukubali kurudi Simba unatoa taswira kuwa baadhi ya mambo yatarekebishwa na kila mmoja atawekeza nguvu zake katika lengo husika. Sifikiri kama kitendo cha Phiri kurudi nchini kitainusuru timu hiyo zaidi ya Simba wenyewe kujifunza na kurekebisha makosa yaliyopita. Phiri alifanya kazi nzuri kweli kweli, alitengeneza timu imara akitumia wachezaji wazawa na wale wa kigeni wenye ubora, ila atafukuzwa kama atashindwa kuirejesha timu hiyo katika nafasi za juu msimu ujao.

Post a Comment