0

AJIBU (ALIYEPIGA MAGOTI) AKISHANGILIA NA WENZAKE BAADA YA KUFUNGA MOJA YA MABAO...


JUZI Jumatano usiku, Simba ilipata ushindi mnono wa mabao 4-0 dhidi ya Taifa Jang’ombe na kutinga kwa kishindo katika hatua ya Nusu Fainali ya Kombe la Mapinduzi inayoendelea kisiwani Zanzibar.


Mchezaji chipukizi katika kikosi cha Simba, Ibrahim Ajibu aliyeingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Awadh Juma na kutupia mabao matatu ‘hat trick’ kisha Shaban Kisiga kufunga moja, amekuwa gumzo kila kona.

Ajibu ambaye mashabiki wa Simba wanaamini ndiye Haruna Moshi ‘Boban’ mpya kikosini hapo, alionyesha kiwango kikubwa katika mechi hiyo kiasi cha kuwatisha wapinzani wanajiandaa kukumbana na Simba.

Mchezaji huyo mwenye majina mengi ya utani yakiwemo Ibracadabra, Mido na Milito, amezungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum, jana Alhamisi, akatiririka:

Ulijisikiaje kufunga hat trick?
Nilijisikia furaha mno kuona naingia uwanjani timu ikiwa haina matokeo lakini nakwenda kuwa chachu ya ushindi, ni jambo zuri zaidi kwangu kwenye historia ya maisha yangu ya mpira.

Kocha alikwambia nini ulipokuwa unaingia?
Wala hakuniambia maneno mengi, alitunyanyua tu kwenye benchi mimi na Simon (Sserunkuma) akatuambia kuwa mechi imeshakuwa ngumu na ninyi ndiyo tegemeo langu la mwisho kwa ajili ya kubadili matokeo, basi tukaingia na Mungu akasaidia kweli tukabadili matokeo.

Ukiwa uwanjani unajiamini sana, siri ni nini?
Yaani hakuna kitu kingine zaidi ya kujiamini, ndiyo maana huwa nafanikiwa mara nyingi.

Nafasi ipi unamudu zaidi uwanjani?
Nashukuru nimejaaliwa uwezo wa kucheza nafasi zote za kiungo mshambuliaji kuanzia pembeni mpaka katikati lakini nafurahi zaidi nikicheza namba 10.

Vipi kuhusu ushindani wa namba?
Ushindani upo lakini naamini nitacheza kwenye kikosi cha kwanza muda si mrefu kwa kuwa kocha aliyekuja sasa (Goran Kopunovic) amesema anampanga mtu kutokana na bidii yake.

Nani alikuleta Simba?
Mara ya kwanza bro Patrick (Rweyemamu, Meneja wa Simba B) ndiye alinikaribisha nijiunge na Simba B kama miaka minne hivi iliyopita baada ya kuniona kwenye moja ya ‘game’ zangu za uswahilini. Baadaye niliondoka na hivi karibuni nikaitwa tena.

Nani aligundua kipaji chako?
Namshukuru sana mama yangu, kwani ndiye aliyekuwa akinishikilia sana na kunipa sapoti katika ishu zangu za mpira, yupo Uarabuni lakini amekuwa anikiunga mkono kwa kila nachokifanya.

Unafikiri Kopunovic atarejesha heshima ya Simba?
Namwamini sana huyu mwalimu, ana falsafa zake ambazo naamini zitasaidia sana kuijenga timu na kukaa kwenye mstari.

Taji la Kombe la Mapinduzi litatua wapi?
Nina imani kubwa tutalibeba kombe kwa sababu katika timu zilizobaki, zote tunaweza kupambana nazo na pengine hata kuzishinda na kutimiza azma yetu.

Vipi kuhusu ufungaji bora?
Ni kweli Msuva (Simon wa Yanga) ana mabao manne, yupo juu yangu kwa bao moja lakini kama nitapata nafasi katika mechi zilizobaki, nitajitahidi kufunga kadiri ya uwezo wangu kisha mwisho wa mashindano tutajua nani kafanikiwa.

Ulianzia wapi soka?
Nilianzia soka la ushindani katika ile timu ya Boom FC ya Ilala kwenye Ligi Daraja la Pili na la Kwanza, nikaenda Simba B baadaye nikatimkia Mwadui ya Shinyanga na msimu huu ndiyo nimetua Simba.

Ndoto zako zipoje?
Ningependa siku moja niwe mchezaji wa soka la kulipwa nje ya nchi.

SOURCE: CHAMPIONI

Post a Comment

AddThis

 
Top