0
SIMBA ni moja ya timu chache nchini ambazo zinasifika kutoa nafasi kwa wachezaji vijana ambao baadaye wanakua na kuwa tishio.


Kuna mipango ya wachezaji wengi na katika kikosi cha sasa wapo Said Ndemla, Jonas Mkude na Ramadhani Singano ‘Messi’.

Hata kama haikuwakuza tangu mwanzo, Simba imekuwa ikithamini vijana. Kikubwa ni utoaji wa nafasi.

Ibrahim Ajibu ni kati ya wachezaji makinda wanaokipiga katika kikosi cha Simba. Nimeambiwa ana umri wa miaka 20.

Bila kujali anashiriki, kapunguza mmoja au miwili, ukweli ni kwamba Ajibu ni kati ya wachezaji wenye kipaji cha juu sana.

Nilianza kumuona katika mechi kadhaa za kirafiki Simba ilizomtumia. Niliona mambo kadhaa ambayo hayahitaji kocha mkuu wa timu kuyang’amua.

Kwanza kipaji cha umiliki mpira, kasi, maamuzi ya haraka lakini ukweli mkubwa wa kupiga mashuti nje ya eneo la 18.

Siku niliyotaka kujua zaidi kuhusiana naye ni mechi ya kirafiki wakati Simba ilipoivaa Gor Mahia ya Kenya na kushinda kwa mabao 3-0.

Ajibu ambaye wakati huo alikuwa amesokota rasta ndogondogo kichwani, aliingia katika kipindi cha pili na kuonyesha uwezo mkubwa.

Wengi pia walitaka kumjua ingawa alifunikwa na Mkenya Paul Kiongera ambaye alifunga mabao mawili dhidi ya timu ya zamani.

Baada ya kumuulizia nikitaka kujua alikopitia kisoka, ajabu taarifa za kwanza zilikuwa ni kuhusiana na utukutu wake. Sikuzitaka sana hizo, ila nilifurahi kuzifahamu.

Zaidi nikasisitiza kutaka kujua alikopitia. Nimeelezwa aliwahi kung’ara na Boom ya Ilala, alifanya mazoezi na Ashanti United lakini hakusajiliwa na baadaye akajiunga na Simba B ambayo ilikubali kumuachia akaenda Mwadui FC kabla ya kusajiliwa Polisi Moro ambayo hata hivyo hakuichezea, akarudi Simba.

Hizo zote ni hadithi, lakini muhimu ni mambo mawili makubwa. Simba kukubali kumpa nafasi yeye na vijana wengine, pia uwezo alionao na majibu ya kuwa Watanzania wanaweza kutafuta viungo washambuliaji bora hapa nyumbani na si kuangalia Kenya na Uganda pekee.

Baada ya jana kufunga mabao matatu wakati Simba ilipoilipua Taifa ya Jang’ombe kwa mabao 4-0 katika mechi ya Kombe la Mapinduzi, Ajibu anatoa majibu kwamba kuna vijana wengi wa Kitanzania kama ilivyo kwake wana uwezo mkubwa lakini nafasi si ya kutosha.

Kuna kila sababu ya kuanza kuamini vipaji vya soka hapa nchini ni rundo na Ajibu ni sehemu ndogo tu ya vijana hao. Basi kuwe na utaratibu maalum wa kuwapa nafasi na kukubali wanaweza.

Azam FC pia wamekuwa wakijaribu, tumeona yule kinda Mudhatir Yahya sasa ndiye anacheza kiungo na Azam FC haitetereki licha ya kumkosa Kipre Balou, raia wa Ivory Coast.

Ajibu alifunga mabao mawili dhidi ya Mwadui, kwa mabao hayo matano ukijumlisha yale ya jana. Ni sehemu tosha ya kuthibitisha kipaji na uwezo alionao. Hivyo apewe nafasi zaidi.

Kwake Ajibu, kama kweli ni mtukutu kama nilivyohadithiwa, basi nimuwahi mapema. Kwamba kwa uwezo alionao na Simba wakiendelea kumpa nafasi naye akajituma, hakuna ubishi atatoka.

Basi kama atafanikiwa, ili kuonyesha yeye na vijana wengine wa Kitanzania wanastahili kupewa nafasi zaidi, basi asivimbe kichwa na baadaye kuonekana ni mfano mbaya wa kujisahau mapema ili kuwapa tiketi wale wanaoamini wageni ndiyo kila kitu, kuendelea ‘kuwaabudu’.

Post a Comment

AddThis

 
Top