Wakati Carlos Alberto Perreira alipomjumuhisha, Ronaldo De Lima katika kikosi cha wachezaji 23 wa Brazil kwa ajili ya fainali za kombe la dunia nchini Marekani, 1994 wengi walishangazwa na maamuzi hayo kwa kuwa mshambuliaji hatari, Geovan Elber aliachwa. Carlos alifanya hivyo si kwa maana ya kuvunja rekodi ya Pele ‘ mfalme wa kandanda duniani’ ambaye alifunga mabao sita katika michezo saba ya fainali zake za kwanza za kombe la dunia akiwa na miaka 17 nchini Sweden, 1958.
Ronaldo alikuwa ametoka kufunga mabao 65 katika michezo 65 akiwa na klabu ya Cruzeiro, Perreira aliamua kumjumuhisha kikosini kwa lengo la kumuongezea uzoefu wa michuano hiyo mikubwa kwa sababu kikosi alikuwa na washambuaji bora huku mwanasoka bora wa dunia akiwemo. Romario De Souza, Bebeto ilikuwa safu kali ya mashambulizi ambayo iliwapatia, Selecao taji la nne la dunia katika bara la nne tofauti. Ronaldo alifunga mabao manne katika fainali za Ufaransa, alicheza mechi zote saba ikiwemo ya kichapo kutoka kwa wenyeji Ufaransa katika mchezo wa fainali ambao Brazil ilichapwa mabao 3-0.
Mabao nane katika michezo saba mwaka 2002 katika fainali za Korea Kusini na Japan yalimfanya ‘ El Phenomeno’ kuifikia rekodi ya Pele ambaye alifunga mabao 12 katika fainali nne alizowahi kuichezea Brazil katika miaka ya 1958, 1962, 1966 na 1970 . Brazil ilishinda taji lake la tano na la mwisho kwa kuilaza Ujerumani kwa mabao 2-0, mabao yote yakifungwa na Ronaldo. Ronaldo akiwa ‘ mwenye umbo kubwa’ alifunga mabao manne katika zake za nne na za mwisho nchini Ujerumani. Licha ya Brazil kuondolewa katika robo fainali na Ufaransa, Ronaldo alifanikiwa kuvunja rekodi ya mabao ya Mjerumani, Gerd Mueller ambaye alikuwa na mabao 15 tangu mwaka 1978.
Ronaldo alifikisha mabao 16 katika michezo 19 ya fainali za kombe la dunia. Mjerumani, Miloslav Klose ametumia michezo 23 kuvunja rekodi hiyo ya Ronaldo baada ya kufunga mabao 17 katika fainali nne za michuano hiyo. Klose alifunga bao la 17, katika mchezo wa nusu fainali ambao Brazil ilifungwa mabao 7-1 na Ujerumani, Julai iliyopita. Ronaldo alikuwa mshambuliaji bora zaidi wa mwisho kuwahi kutokea Brazil, alifunga mabao 67 katika michezo 97 ya Brazil katika kipindi cha miaka 12 ya maumivu ya muda mrefu.
Ronaldo alitingisha barani ulaya akiwa na PSV, Barcelona, Inter Milan. Real Madrid na kiasi fulani alifanikiwa katika kikosi cha AC Milan. Wakati akitamba, Brazil ilikuwa ikianza kushuhudia mafanikio ya wachezaji wao barani ulaya. Romario alitwaa tuzo ya dunia mwaka 1994 akiwa na Barcelona, aliondoka PSV kumpisha Ronaldo, na alimpisha tena klabuni Camp Nou miaka miwili baadae wakati, Sonny Anderson akichukua nafasi ya Ronaldo pale PSV. Wakati huo soka lipo, Uholanzi, Italia, Ujerumani na Hispania.
Wabrazil walitamba klabu kubwa huku wakiachana nafasi. Ronaldo alipoondoka Barca na kujiunga na Inter Milan ya Italia kwa usajili wa rekodi ya dunia, Sonny alichukua nafasi ile pale Barca. Miaka mitatu tangu kustaafu soka la ushindani kwa Ronaldo, Brazil haina mshambulizi wa hatari, licha ya kujitokeza kwa Adriano Leite, Luis Fabio, Fred, Selecao wanaweza kumtazama zaidi kijana wa miaka 21, Neymar kama mchezaji ‘ alama’ ya vipaji vya Wabrazil duniani. Neymar amekuwa mfungaji hasa, alifunga katika mchezo ambao Barcelona walibanwa kwa muda wote na Bilbao wikiendi iliyopita.
Lakini upande mwingine kuna wachezaji ‘ Wabrazil’ wamedhihirisha umahiri wao katika ufungaji wa mabao. Diego Costa alifunga ‘ hat-trick’ ya kwanza katika mchezo wa nne wa ligi kuu England huku akifikisha idadi ya mabao saba na kuwa kinara wa chati ya ufungaji bora. Geilson Santos ‘ Jaja’ alifunga mara mbili katika mchezo wake wa kwanza wa mashindano akiwa na Yanga huku akifikisha mabao manne katika michezo mitano tangu atue Yanga. Ulimuona Costa wakati akizipokea pasi katika mchezo dhidi ya Swansea? Ulimuona Jaja alivyotulia na kujiamini kisha akapiga mpira kiufundi dhidi ya Azam FC? Hawa ni Brazil tu, labda wapinzani wawape heshima yao. Wataendelea kufunga kama hawatapata majeraha.


Post a Comment